Quality Education for Quality Life

Sunday, December 27, 2015

MARAFIKI WA AFRIKA MASHARIKI (DENMARK) WATEMBELEA SEKONDARI YA LUSHOTO KUPATA MREJESHO WA UFADHILI WA MIRADI YA KITAALUMA




Marafiki wa Africa Mashariki – Denmark ni jumuiya ya watu wenye kusaidia jamii za afrika mashariki hasa katika shughuli za kijamii kama elimu, afya na maji. Marafiki hawa kwa hapa tanzania, wameweza kufanya ushirika wa kusaidia taasisi mbalimbali katika mkoa wa Tanga, nazo ni:
  • Hospitali ya Shifaa Charitable, 
  • Shule ya awali Comfort, 
  • Kituo cha afya Malindi, 
  • Shule ya sekondari Kongei na 
  • Shule ya sekondari Lushoto. 
Jumuiya hii iliundwa mwaka 2007 na hadi sasa ina wanachama tisini (90), ambao wengi wao ni wa asili ya Afrika. Wanachama wengine ni wa asili ya ki – denmark ambao nao hukaa kwa muda mfupi na wengine kwa muda mrefu, sehemu ya Afrika Mashariki (hasa Tanzania, Uganda, Rwanda, Kenya na Burundi) ambapo wanakuwa wakihusiana zaidi na miradi mikubwa na midogomidogo. >>>>>WATEMBELEE HAPA

Dada Fadhila Challange pamoja na marafiki wa Africa Mashariki - Denmark wakiwa na mkuu wa shule Mr Yona Ndekirwa, wakikagua maendeleo na matumizi ya samani zilizopokelewa shuleni kutoka kwa Marafiki.

Katika shule ya sekondari lushoto, Marafiki hawa wamekuwa na mahusiano mema na yenye tija katika kuboresha na kuinua taaluma hapa shuleni. Urafiki na Ushirikiano huu umewezesha kupatika kwa samani za kisasa ambazo zinatumika hapa shuleni na kwa kiasi, tatizo la uhaba wa samani limepungua. Pia shule imepata seti za kutosha za komputa, hivyo kuwezesha katika ufundishaji, ujifunzaji na ufanisi wa shughuli za kila siku za kiutawala.

Katika ziara yao mwezi desemba, 2015; Maraafiki wameweza kufanya mahojiano na wanafunzi kadhaa pamoja na walimu wao ili kujua '' ufadhili na urafiki baina ya shule na nchi ya Denmark (Marafiki wa Afrika Mashariki), umetumikaje, umeleta tija na manufaa gani kwa jumuiya kusudiwa ya sekondari lushoto; aidha pia kufahamu mahitaji na changamoto zinazoikabili shule. Kwaniaba ya wanafunzi wote wa sekondari lushoto; hawa waliwasilisha maoni na shukrani zao za dhati kwa Marafiki wa Afrika Mashariki.

ANDREW FRANK (Mwanafunzi kidato cha tatu , 2015):
Akiwa kidato cha pili hapa sekondari ya lushoto, alianza kujifunza kutumia komputa; na kujua mambo mbalimbali yaliyomsaidia katika uelewa na ufaulu wa masomo yake. Andrew, F. ana ndoto za kuwa mfanya biashara mkubwa ambaye atatumija ujuzi na maarifa ya komputa kuendesha biashara zake, pia kusaidia wengine kama wafanyavyo Marafiki wa Afrika Mashariki. >>>>> TAZAMA VIDEO YAKE

SHARIFU RAMADHANI (Mwanafunzi kidato cha tatu, 2015):
Kutokana na manufaa ya urafiki, yeye anatoa shukrani za dhati kwa shule na Marafiki wa Afrika Mashariki; kwa kupata komputa na thamani za kuwawezesha kujifunza teknolojia mpya na ya kisasa kupitia vifaa hivyo. Sharifu, R. hutumia komputa hasa katika kujifunza mada za somo la bailojia, kujitafutia maarifa na ufahamu zaidi. Mfano ameweza kujifunza kwa ufasaha zaidi mada ya ''locomotion'' katika komputa hizo. >>>>> TAZAMA VIDEO YAKE

HATIKI SHERIMO (Mwanafunzi kidato cha tatu, 2015):
Tangu akiwa kidato cha pili hapa sekondari lushoto, ameweza kujifunza kutumia komputa. Anakiri kuwa, uwepo na kujifunza matumizi ya komputa kumemsaidia sana kitaaluma; masalani yeye hutumia zaidi kamusi ya jiografia iliyoko katika komputa hizo ili kutafasiri msamiati anaokumbana nao katilka masomo yake, na kujiongezea ufahamu zaidi. >>>>> TAZAMA VIDEO YAKE

ASHA MOHAMED (Mwanafunzi kidato cha tatu, 2015):
Akiwa kidato cha tatu, ndipo alipopata wasaa na fursa ya kuijifunza na kutumia komputa. Mada ya somo la jiografia - '' Earthquake'' ameielewa kwa mapana yake baada ya kupata maelezo ya ziada (kwa picha, maandishi na video) zilizopo katika komputa za shule. Mbali na kujifunza darasani, Asha, M. ametenga muda wa ziada ili kujifunza zaidi kwa msaada wa komputa zilizopo shuleni.>>>>> TAZAMA VIDEO YAKE 

ZAWADI HEMEDI (Mwanafunzi kidato cha tatu, 2015):
Mwanzoni alikuwa hafahamu chochote kuhusu komputa , zaidi ya kusikia tuu. Uwepo wa vifaa hivyo (komputa) hapa shuleni; ni fursa nzuri kwa Zawadi, H. na wanafunzi wengine kuziona, kujifunza na kutumia ili kujiongezea maarifa na kuwa wasomi wa kisasa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia.

AISHA WAZIRI OMARY (Mwanafunzi kidato cha tatu, 2015): Kujifunza kutumia komputa; kumempatia maarifa ya mambo mengi ya kitaaluma na ufahamu wa masuala mbalimbali. Aisha, W. O. anatoa neno kwa wanafunzi wenzake, '' ni vyema wanafunzi kujifunza kutumia komputa ili kujiongezea wigo wa kuelewa mada wanazojifunza darasani ''.  >>>>> TAZAMA VIDEO YAKE

MR. SWALEHE A. MSANGI (Mwalimu – Taaluma lushoto sekodari): ''Ushirikiano huu wa lushoto sekondari na Marafiki wa Afrika Mashariki - Denmark , ni mzuri na una matunda mema yenye manufaa hasa kwa maendeleo ya wanafunzi kitaaluma''. >>>>> TAZAMA VIDEO

MR PETER R. MSHAHARA (Mwalimu – Mhifadhi na mgavi lushoto sekondari): ''Manufaa ya misaada na miradi hii ya kitaaluma shuleni (inayotokana na ushirikiano baina ya lushoto sekondari na Marafiki wa Afrika Mashariki – Denmark) ina thaminiwa na imeleta tija zaidi si kwa wanafunzi pekee, bali kwa walimu na jumuiya ya shule pia. Kupitia urafiki huu, shule imepata samani (furnitures) kama vile viti, meza na makabati. Vilevile shule imepata seti za komputa na vifaa viambata vyake vingine, ambavyo vyote hutumika katika kujifunzia na kufanya kazi za kiutawala. Walimu nao hutumia fursa hii, kujiongezea maarifa ya kiutendaji kupitia komputa hizi''.
Hivyo jumuiya yote ya sekondari lushoto (walimu,wanafunzi na wazazi), inatoa shukrani za dhati kwa Marafiki wa Afrika Mashariki – Denmark, kwa ushirikiano huu ambao kwa shule umeleta tija, nuru na mwamko zaidi kujiimarisha kiutendaji na kuandaa vijana kitaaluma ili kuendana na mabadiliko na maendeleo ya sayansi naa teknolojia, hivyo kuwa na ujuzi na maarifa stahiki. Tunathamini na kuutunza urafiki huu pamoja na vifaa tulivyo patiwa, ili udumu na kustawi maradufu. 

Tunasema AKSANTE (TAKKE) 

0 comments:

Post a Comment